Mnafiki!
uwongo wako!
hata kama ni kweli
ulipigania uhuru
hata kama ni hakika
ulikuwa kwa Jeshi la Uhuru na Mashamba
hata kama ulisema nini na kufanya kitu gani
dhidi ya ukoloni-mkongwe
ikiwa sasa wewe ni msaliti
ikiwa wakati huu u kibaraka cha mabeberu
ikiwa leo wewe ni mnyonyaji
kama u mbakuzi wa mashamba na maploti
endapo unaunga mkono mfumo wa unyonyaji wa mtu kwa mtu
ikiwa unadai kuna uhuru Kenya leo
hakika kabisa wewe si shujaa wa wananchi
wala usifikiri u mzalendo hata kidogo
kwani ulafi wako
tamaa ya mali na pesa
ubinafsi
unafiki na ubarakala wako
umefuta historia yako safi ya jana
kweli huwezi kutudanganya tukadanganyika
wala huwezi kusema tukakusikiliza
katika historia ya leo ya nchi yetu
wewe si rafiki wa mapambano ya ukombozi wa kijamii
leo umegeuka kuwa adui, unapinga maendeleo ya nchi yetu
kwa kuwa umekubali kuwa mbwa wa wakoloni-mamboleo
kwa sababu unazungumza lugha ya wagandamizaji
madhali unatetea mfumo wa ubepari
maana leo u fisi na nguruwe
maadamu sasa u sawa na kupe na kunguni
kwa vile u malaya mkubwa siku hizi
shujaa wa kweli wa umma
mzalendo halisi
husafiri hadi mwisho wa safari
na safari yetu ya mapambano bado ingaliko
haijafika mwisho wake safari yetu ya uhuru na maendeleo
kwani ukoloni-mamboleo ungaliko katika nchi yetu
wananchi tunaumizwa na udikteta wa kanu
ingawa bendera inapepea uhuru wenyewe bado
kumbe wewe ulikuwa ukipambania tumbo lako tu
kumbe nia yako ilikuwa kuchukua nafasi ya mkoloni
tulikataa unyonge wa kunyanyaswa na Waingereza
unafikiri tutaikumbatia aibu
ya kudhulumiwa na Wafrika wenzetu?
shetani mkubwa wewe!
msaliti unaechafua jina safi la Mau Mau!
mzandiki!
Mwandawiro Mghanga, CPK, Jela Kuu ya Kibos 25-02-1988







