Ni Siku Kuu ya Afrika, Wafrika tuishangilie
Tujitakie heri baraka, ili uhuru utufikie
Uhuru bado haujafika, tuungane tupambanie
Na ili ukombozi kufika, itabidi kazi tufanyie
Afrika tuishangilie, ni Siku Kuu ya ukombozi
Ni Siku Kuu ya Ukombozi, ya kukumbuka historia
Tusisahau hata machozi, hayo Wafrika tulilia
Walitukuta tukila ndizi, utumuani wakatutia
Wakatutoa bara mzazi, huko mbali kutuhamishia
Tukawajenga na zetu kazi, pia kwa mali kutuibia
Machungu mno tulipitia, kuliko wengine duniani
Halafu ukaja ukoloni, ukaivamia Afrika
Wakatudhulumu wakoloni, wakitupora na kutubaka
Tukatajirisha Uzunguni, Afrika tukafukarika
Tukavurugiwa tamaduni, ada zetu kusambaratika
Tukatupa za kijadi dini, zile za kigeni tukashika
Leo tukumbuke Wafrika, hata pia sisi binadamu
Tumepitia mengi magumu, histori yetu si rahisi
Na kukitia kidonda sumu, bado ingali yao mikosi
Ubeberu ungaliko humu, bado wazidi kutufilisi
Mirija ya kutunyonya damu, walinda viongozi mafisi
Waliyotupa ubinadamu, hao ndiyo watawala sisi
Ni ndugu zetu watu weusi, wapingao wetu ukombozi
Wahujumuao ukombozi, hasa vijana nisikizeni
Kwa kweli ni hao mabazazi, wanaoshikilia sukani
Na Afrika kote ni wazi, kasoro iko uongozini
Basi vijana ni kwenu kazi, jukumu lenu litambueni
Uhuru ni lazima mapinduzi, jizatitini kazi anzeni
Kila juhudi tuifanyeni, Afrika tukaikombuo
Afrika tukaikombuo, tuondoe hiyo mipaka
Vikwazo vyote tuvifunguo, tusibaguane Afrika
Nisafiri bila usumbuo, Mwafrika huru Afrika
Na ubepari tuupenduo, ukamalizike Afrika
Ujamaa ni maendeleo, tuupambanie Afrika
Siku Kuu ya Afrika, ujumbe huu nafikisha
Ujumbe huu nafikisha, Siku Kuu ya Afrika
Na vita ni lazima kuisha, twataka amani Afrika
Tuwe wa kuyajali maisha, tukuze ungwana Afrika
Pia imla lazima kuisha, watu wawe huru Afrika
Na ufisadi uwe ni kwisha, haki ikanoge Afrika
Ni Siku Kuu ya Afrika, Wafrika natuzindukeni
Wafrika natuzindukeni, tuna mali nyingi Afrika
Tukumbuke bado ukoloni, Sahara Magharibi Afrika
Wasahara Magharibi jamani, tuwakomboe ni Wafrika
Na kambi jeshi za wakoloni, tuzitoe kwetu Afrika
Na liwe ni bara la amani, tuwe na salama Afrika
Ni Siku Kuu ya Afrika, tuitilie kweli manani
Mwandawiro Mghanga, Mwenyekiti wa SDP
Nairobi, Jumatano, Mei 25, 2015







