Siku Kuu ya Mashujaa wa Uhuru
Ilikuwa tarehe 20 Oktoba na mwaka ni wa 1952
Wakoloni walipoamua kuzidisha njama zao
Za kuwavamia wazalendo wana halisi wa taifa letu
Waliyokuwa wameamua kujitolea kuutetea utu wa mtu mweusi
Wakizunguka kote nchini kutangaza mapambano ya uhuru
Huku wakifichua wasaliti vibaraka wa wakoloni
Na kiapo wakilishana kiapo chenyewe cha kuapa
Kenya ni nchi ya Wakenya Wazungu warudi kwao
Tunapigania uhuru na ukombozi tunadai mashamba yetu
Ni haki yetu kujitawala tunataka kujiamulia sudi yetu wenyewe
Ila haki hatutapewa kama zawadi na wakoloni
Itatupasa kuipigania kwani uhuru utadai hata damu yetu
Kwa hivyo tujizatiti tuwe tayari kwa vita vigumu na vikali
Wala hatutorudi nyuma tutapigana mpaka tutakapojikomboa
Wakoloni wakasikia kuhusu kiapo cha kuwaunganisha wadhulumiwa
Wakaogopa sana wakatetemeka kwa hofu na dukuduku
Sauti madhubuti ya wananchi ikautingisha ukolonimkongwe
Serikali ya kikoloni na walowezi na machifu na mahomugadi wote
Wakashindwa kutawala kunyonya na kusaliti kwa amani
Wakawa wanasaka wanakamata wanafunga wanaweka vizuizini wazalendo
Viongozi wa mapambano ya uhuru wasiweze kulala majumbani mwao
Kifagio cha polisi na askari kanga kikakusanya wananchi kwa maelfu
Hali ya hatari ikatangazwa maanake vita moto dhidi ya Wakenya wote
Nyakati za ufashisti wa Wingereza dhidi ya taifa letu
Zikatangazwa rasmi na dola la ukoloni nchini kwetu
Njia zote za kudai uhuru kwa amani zikafungwa kabisa zikazibwa rasmi
Ndipo kibirikizi kikalia wazalendo wakakusanyika
Wafanyikazi na wakulima wa Kenya wakasema wakati umewadia
Sisi pia ni binadamu wenye akili na damu kama wao
Kwa vile tunakufa hatutoendelea kukubali kufa kikondoo
Maana wameamua kutuchinja tunakataa kuzidi kuchinjwa kama nguruwe
Tunasema potelea mbali dawa ya moto ni moto
Mwenye bunduki aanze kupiga na wa bomubomu alipue
Wa panga atoke na panga na wa mkuki na mkuki wake
Masogora wa vita wakati wa kuonyesha ufundi wenu umefika
Kuanzia hivi leo ni kufa ama kupona hadi ukombozi wa taifa letu
Maadui ni wakoloni walowezi na machifu na mahomugadi wao
Jeshi la Uhuru na Mashamba likatangaza vita vya kigorila
Umashuhuri wa Mau Mau ukaanza kuenea nchini na duniani kote
Basi tukumbuke siku hii si ya mahomugadi wa jana na leo
Si siku ya waoga na wasaliti walotumiwa na adui dhidi yetu
Si siku ya serikali inayoukumbatia na kuubusu ukolonimamboleo
Si siku ya wanyonyaji na wabakuzi wa mashamba na maploti
Wala si sahihi kuiita Kenyatta Dei aliyekufa akiwa msaliti mkuu
Ni siku kuu ya kitaifa ya kuwakumbuka mashujaa wa uhuru
Ni siku ya Jeshi la Uhuru na Mashamba siku kuu hii ni ya Mau Mau
Ni siku ya kutukumbusha uhuru wa kitaifa hudai kujitolea mhanga
Na kwamba ukombozi bado kwani ukolonimamboleo ungaliko
Ushahidi wake ni kwamba hivi leo tuko gerezani
Siku kuu hii
Kwa mara nyingine tena
Ninalazimika kuisherehekea jela
Mimi na wazalendo wengine
Siku Kuu ya Mashujaa wa Uhuru
Tunaikumbuka tukiwa wafungwa wa kisiasa
Tuko gerezani wakati huu
Kwani tunaitikia mwito wa mashujaa wa uhuru:
Pambana siku zote pambana!
Pambana hadi ukombozi kamili wa kijamii na kitaifa!
Mwandawiro Mghanga
Jela Kuu ya Kibos Oktoba 20 1988
Tuwakumbuke Mashujaa Wetu
Tuwakumbuke
Mashujaa wa nchi yetu
Wazalendo halisi wa Kenya
Jinsi walivyokuwa wamejitolea mhanga
Kupambania uhuru na ukombozi wa nchi yetu:
Na sisi leo
Lazima tupambane kwa vyovyote vile
Tujikaze kisabuni
Mateso na majaribu ya kila aina
Tunayaona
Na tutaendelea kuyaona
Tuwakumbuke mashujaa wa Pwani ya nchi yetu
Wazalendo wa Mombasa na Malindi na Lamu
Na Siu na Pate na Vanga
Ambao mamia ya miaka iliyopita
Walikufa wakipambana
Wakipambana dhidi ya uvamizi wa Waarabu
Waliyokataa kutawalwa na wageni
Waliyoupiga vita uvamizi wa kikatili wa Wareno
Wareno wakashindwa kabisa kupenya hadi bara
Tukumbuke kuwa ngome
Inayoitwa Fort Jesus
Ambayo sasa ni jumba la ukumbusho Mombasa
Ngome ni taswaira ya uvamizi wa Wareno nchini
Ni ushahidi wa upinzani kutoka kwa mababu na mabibi zetu
Ni ukumbusho wa nyanyaso na gandamizo
Za Wazungu wa kwanza kujaribu kutawala Kenya
Ngomeni maelfu ya Wamijikenda na Waswahili walifungwa
Ngomeni wazalendo wa nchi yetu waliteswa
Ngomeni damu ya mashujaa ilimwagika
Tumtaje Shee Mvita, mfalme wa mwisho wa Mombasa
Aliyeuawa na Wareno
Akiutetea uhuru na ukombozi wa watu wake
Mfano wa bei ghali iliyolipwa na wazalendo
Na sisi leo
Lazima tupambane kwa vyovyote vile
Tujikaze kisabuni
Mateso na majaribu tilatila
Tunayaona
Na tutaendelea kuyaona
Mwangeka
Wawa Mwangeka wa Mwanda Njawuli
Mzalendo kutoka Vuria
Kilele cha milima ya Dawida
Milima ya juu zaidi Mashariki mwa Kenya
Inayosifika kwa uzuri wake usiyo na kifani
Kule kulikopandishwa bendera ya uhuru wa Kenya Pwani
Ing'oni Mwangeka mzaliwa sehemu hii ya nchi yetu
Naye anatajika, ni mtu mashuhuri
Kwa uzalendo na ushujaa
Kwa kuongoza maaskari hodari wa Dawida
Waliyowaeleza wakoloni kwa mikuki, nyuta na mishale
Nyinyi ni nani mnaotamba katika nchi yetu?
Hii ni ardhi yetu kutoka kale na zamani
Tutaitetea hata kwa damu kumwagika
Tunapinga kutawalwa na wageni
Tuko kwa nchi yetu tunawezaje kuwafanyia kazi?
Tunaishi kwa jasho letu wenyewe
Basi itakuwaje tuwe wapagazi wenu?
Tu watu kama nyinyi tutakubalije kuwa watumwa wenu?
Tuna lugha, dini, mila na tamaduni zetu hatuna haja na zenu!
Kina Mwangeka wakatangaza vita dhidi ya vita vya wakoloni
Wakapigana wakapigana wakapigana bila kurudi nyuma
Mwangeka na maing'oni wa Dawida
Wakakataa kufa wakipiga magoti
Wakadinda kuwainulia maadui mikono yao
Wakafa wakiwa na silaha mikononi
Na sisi leo
Lazima tupambane kwa vyovyote vile
Tujikaze kisabuni
Mateso na majaribu tilatila
Tunayaona
Na tutaendelea kuyaona
Halafu kuna Me Kitilili
Me Kitilili Me Kitilili Me Kitiliii
Me Kitilili wa Menza
Me Kitlili mwanamke shujaa kutoka Ugiriamani
Mzalendo Me Kitilili na Wanje, Wanje wa Mwadorikola
Jazanda ya uzalendo wa wanawake wa nchi yetu
Waliyowaongoza wanaume na wanawake wa Ugiriamani
Kuuasi na kuulani ukoloni kwa maneno na vitendo
Kukataa kuwa maaskari wa wakoloni
Kugoma kufanywa mahamali wa mabeberu
Kudinda kunyang'anywa ardhi yao
Wakoloni wakawashambulia kikatili kikoloni
Wanje wa Mwadorikola na Mee Kitilili
Wakawaongoza wanaume kwa wanawake
Kutetea mila na tamaduni za Wagiriama
Kulinda hadhi ya mtu mweusi, heshima ya Mwafrika
Wakoloni wakawaita wanawake mashujaa wetu wachawi
Wakakashifiwa wakakamatwa wakadunishwa wakateswa
Mama zetu wakahamishwa hadi nchi ya Wakisii
Bali Me Kitilili na Wanje wa Mwadorikola
Wakasimama madhubuti wasitingishike wasikate tamaa
Wakatoroka na kujasiri mamia ya kilometa
Wasiogope hatari za nyika na misitu na wanyama tilatila
Wakarudi Ugiriamani kuendelea na mapambano
Wakaendelea kuongoza harakati dhidi ya ukoloni
Wakatukanwa wakapakwa matope wakazuiwa wakafungwa
Wakahamishwa hadi Kisimayu
Bali mama zetu milima ya ushujaa na uzalendo
Mfano wa ukakamavu na kujitolea mhanga
Wakakataa kusalimu amri za wakoloni
Wakatetea uhuru wa nchi yetu na watoto wao daima
Wakaishi wakiwa mihimili ya umoja wa watu wao
Wakawa sehemu ya nguzo ya historia ya ukombozi wa Kenya
Na sisi leo
Lazima tupambane kwa vyovyote vile
Tujikaze kisabuni
Mateso na majaribu tilatila
Tunayaona
Na tutaendelea kuyaona
Huko Unandini Koitaleli ni mashuhuri
Koitaleli, kiboko cha kiburi cha wakoloni
Wanandi kwa mikuki na ngao mikononi
Wakawauliza wakoloni:
Hii ni nchi yetu kutoka tangu na tangu
Nani amewaruhusu kujenga reli hapa?
Mnawezaje kuingia na kupita kwetu
Bila hata hodi wala hamjambo!?
Mna njama gani juu ya ardhi yetu
Ambapo tumekuwa tukiishi tangu kale na zamani!?
Wakoloni kwa kiburi kujitapa na kujisahau
Wakajibu kwa bunduki na bomubomu
Kwa kuua na kuchinja pasina kutangaza vita
Wanandi wakatahamaki wakajizatiti sawasawa
Wakasema hawa watu ni wa sampuli gani?
Watu gani hawa wasiyo na utu heshima wala adabu!
Ni binadamu gani hawa wasiyojali maisha?
Hawajui lugha nyingine ila vita na madharau tu?
Basi, imetupasa kupigana nao
Kwani nasi hatuna utamaduni wa woga
Ndipo Wanandi wakajiandaa ipasavyo
Kwa mikuki na ngao wakajumuika
Mabingwa wa vita vya kigorila wakajipanga barabara
Wakawa wanawavizia na kuwashambulia ghaflaghafla wachokozi
Kina Koitaleli wakawachapa wavamizi hadi wakasarenda
Wakatapika kiburi chao wakaomba majadiliano
Mwafrika, mtu mweusi, akawafanya wainue mikono
Ikawa hawana budi ila kuitisha majadiliano ya amani
Ela Koitaleli alipoenda kujadiliana na mabeberu akauawa!
Shujaa Koitaleli akauawa kwa mizungu ya Wazungu ya kioga
Unafiki wa wavamizi ukadhihirika wazi na bayana
Hakika mkoloni si mtu mwaminifu
Bali kina Semoi wakachukua nafasi ya shujaa Koitaleli
Mapambano dhidi ya ukoloni yakaendelea
Na sisi leo
Lazima tupambane kwa vyovyote vile
Tujikaze kisabuni
Mateso na majaribu tilatila
Tunayaona
Na tutaendelea kuyaona
Tunajivunia Waiyaki
Waiyaki Waiyaki Waiyaki
Waiyaki wa Dagoreti
Chimbuko cha mapambano ya Wakikuyu dhidi ya walowezi
Damu iliyozaa Jeshi la Uhuru na Mashamba, Mau Mau
Kina Waiyaki walipinga unyonyaji wa makampuni ya kibeberu
Walisema hapana kwa ubepari nchini
Hapana kwa mfumo wa kiuchumi wa unyonyaji wa mtu kwa mtu
Walivamia ngome za kupanda mizizi ya mirija ya ubeberu Kenya
Wazalendo wa nchi yetu waliasi kupunjwa na wageni
Walidinda kuwa watumwa wa Wazungu
Wakakataa na utu wa Mwafrika kwa silaha
Waiyaki akakamatwa kuhamishwa Pwani
Wakamshawishi wakamtisha wakamtesa ili asarende
Wapi! wakapiga ukuta kwa babu yetu
Wakashindwa kuumwaga uzalendo wa Mkenya halisi
Wasiweze hata kuukwaruza uhodari wake
Ufashisti wa wakoloni ukazidi kudhihirika Kibwezi
Walipomzika shujaa wetu Waiyaki akiwa hai
Miungu ya nchi yetu
Waingereza walimzika mzalendo akiwa bado anaishi!
Na sisi leo
Lazima tupambane kwa vyovyote vile
Tujikaze kisabuni
Mateso na majaribu tilatila
Tunayaona
Na tutaendelea kuyaona
Nyanjiru
Oh Nyanjiru
Tumkumbuke Mary Muthoni Nyanjiru
Yule mwanamke jasiri wa enzi za kiburi cha walowezi
Nyakati za ushujaa wa Harry Thuku
Harakati za wafanyikazi zilipopamba moto
Siku za kukataa kubeba vipande vya wakoloni
Kudinda kulazimishwa kuwafanyia kazi masetla
Kugomea mishahara duni ya kitumwa
Kupinga kunyonywa na kunyanyaswa kwa wanawake
Enzi za chimbuko cha vyama vya kupigania uhuru
Hizo enzi za East African Association
Mapambano ya wafanyikazi katika miji ya nchi yetu
Mapambano dhidi ya kina Colonel Grogan na Lord Delamare
Wakati unyama wa wakoloni dhidi ya wananchi
Ulikuwa ni sehemu ya maisha ya kila siku
Tukitukanwa na kufungwa na kuteswa kiholela
Tukitemewa mate na Wazungu vururumtende
Tukidhihakiwa na kudhalilishwa nyumbani kwetu
Na kina memsahibu walokuwa wakitamba mijini na mashambani
Sisi watu weusi tukifanywa watu wa mwisho
Kana kwamba Kenya si nchi yetu wenyewe
Hizo nyakati za kupinga kulipa kodi kwa wavamizi
Harry Thuku akakamatwa na kuwekwa ndani
Wanaume na wanawake wa Nairobi wakaandamana
Harry Thuku na wafungwa wote wa kisiasa wawachiliwe!
Wafunguliwe mara moja tena bila masharti!
Nje ya Norfolk Hotel
Karibu na Chuo Kikuu cha Nairobi
Si mbali na Central Police Station
Siku hiyo mwaka wa 1922
Kina Nyanjiru walikata shauri kuandamana hapo
Hadi shujaa wao atakapofunguliwa
Hadi Harry Thuku atakapowachiliwa
Wakalala hapo kwa siku na masiku
Baridi ya usiku wakivumilia na njaa na kiu pia
Vitisho vya walowezi wasikubali viwatishe
Bezo za kishenzi za kuuzi za wavamizi wakazipuuza
Na hata wanaume walipozubaa na kusitasita
Walipolegalega na kushindwa kutoa uongozi thabiti
Mary Muthoni Nyanjiru hakulimatia, alijitokeza kimoja
Akadai wanaume wavue surwale na kuvaa skati
Wawape wanawake surwale zao wazivae
Ndipo wanawake wakawa katika msitari wa mbele
Wanaume wakifuata nyuma katika harakati za ukombozi
Pamoja wakasonga mbele kumfungulia mpendwa wao
Pamoja wakaandika historia ya uhuru wetu - kwa damu yao
Shujaa Mary Muthoni Nyanjiru
Akawa wa kwanza kuangushwa na risasi za polisi wa kikoloni
Makaburu waliyokuwa wakistarehe Norfolk Hotel
Huku wakiwatukana na kuwakebehi watu wetu
Wakachukua silaha zao kwa furaha za wehu
Wakaungana na polisi wao kufanya mito ya damu Nairobi
Kutoka kwa mamia ya dada na kaka zetu
Bali yote hayo hayakuuzima moto wa mapambano ya uhuru
Ukaendelea kuwaka moto wa uhuru ukazidi kuzagaa
Na sisi leo
Lazima tupambane kwa vyovyote vile
Tujikaze kisabuni
Mateso na majaribu tilatila
Tunayaona
Na tutaendelea kuyaona
Tumkumbuke Makhan Singh
Komredi Makhan Singh, mkomunisti wa kwanza Kenya
Sehemu ya harakati za wafanyikazi dhidi ya ukoloni
Sogora wa mbinu na hila za kuzatiti mapambano
Mapambano ya wavujajasho dhidi ya mabepari
Katika historia ya vyama vya kimaendeleo vya wafanyikazi
Jina la mwanamapinduzi Makhan Singh litang'aa daima
Makhan Singh, sehemu ya kina Chege Kibacia
Chege Kibacia na mashujaa wa watiririkajasho
Makhan Singh,aliyeaminika hata KAU ya Kiburi House
KAU ya Mau Mau katika Kiburi House
Ndiyo, tusisahau Kiburi House
Kiburi House, walikokuwa wakikutana kina Bildad Kaggia
Kina Eliud Mutonyi na kina Isaac Gathanju
Kiburi House, kulikokuwa kukipangwa njama za Mau Mau
Ngome ya waliyochagua barabara ya mapinduzi
Walimtambua Makhan Singh Kiburi House walimhesabu
Kina Makhan Singh na Pio Gama Pinto na Alibhai Mulla Jeevanjee
Wazalendo wa Kenya wa asili ya Kihindi
Waliyowaambia Wahindi wa Kenya
Enyi wananchi wenzetu wa asili ya India
Tahadharini msiwe mapopo na vinyonga
Epukaneni na kuwa makupe na makunguni wa nchi hii
Ikiwa Kenya ni nchi yenu
Kama mnajihesabu raia wa nchi hii
Unganeni na Wafrika kupigania uhuru wa Kenya
Kuweni sehemu ya wazalendo wanaodai ukombozi
Msikubali kutumiwa kunyonya na kufukarisha taifa hili
Kataaeni kuwa upande wa wakoloni na wadhalimu
Msijidanganye kuwa nyinyi ni bora kuliko wenyeji
Wafanyikazi wote tunanyonywa haya shime tuungane
Tuwe na mshikamano dhidi ya wanyonyaji
Tusikubali ubaguzi wa kimbari utuvunjie umoja wetu
Tuugomee ukabila usitumiwe kuondoa uwezo wetu
Wala tusikubali migawanyiko ya kijinsia iturudishe nyuma
Kenya na Uganda na Tanzania wafanyikazi tuwe kitu kimoja
Wafanyikazi wote tupambanie taifa la Afrika Mashariki
Afrika Mashariki ya kimapinduzi
Afrika Mashariki inayopinga ukolonimamboleo
Afrika Mashariki ya mfumo kwa kisoshalisti
Afrika Mashariki itakuwa nguvu kubwa za kisiasa na kiuchumi
Afrika Mashariki itakuwa matumaini ya uhuru na ukombozi kamili
Sauti ya Makhan Singh, sauti ya wanaonyanyaswa
Iliyoitikiwa na wafanyikazi na umma wa wazalendo
Iliwafanya wakoloni kujikojolea na kujiharia
Makhan aliwakosesha mabepari wa Afrika Mashariki usingizi
Jina lake likaandikwa katika kitabu cheusi cha dola la kikoloni
Na hali ya hatari ilipotangazwa rasmi mwaka wa 1952
Makhan Singh hakusahauliwa na kifagio cha polisi wa kikoloni
Makhan Singh alikamatwa mara moja
Makhan Singh akafungiwa kizuizini
Makhan Singh alifungwa miaka kumi kizuizini
Kwa sababu ya harakati za wavujajasho alifungwa Makhan Singh
Alifungwa kwa ajili ya uhuru wa taifa letu
Bali bendera ya wakoloni iliposhushwa Kenya
Na bendera ya Wakenya kupandishwa
Kupandishwa na mapambano ya kina Makhan Singh
Serikali ya msaliti Jomo Kenyatta na mahomugadi
Ilimchukua Makhan kana kwamba si lolote si chochote nchini
Bali kutambuliwa na wanyapara wa mitaji ya mabeberu Kenya
Kupigana pambaja na wanyonyaji na wagandamizaji wa wafanyikazi
Haikuwa nia ya komredi Makhan Singh, mwanamapinduzi
Makhan Singh alikufa akiandika historia ya mapambano
Historia ya mapambano ya wafanyikazi wa Kenya
Makhan Singh ....Makhan Singh....Makhan Singh.......
Na sisi leo
Lazima tupambane kwa vyovyote vile
Tujikaze kisabuni
Mateso na majaribu tilatila
Tunayaona
Na tutaendelea kuyaona
Mau Mau
Mau Mau, Jeshi la Uhuru na Mashamba
Kilele cha mapambano dhidi ya ukolonimkongwe
Jazanda ya wazalendo na uzalendo
Mau Mau, mashujaa halisi wa nchi yetu
Wakakataa kutembea katika njia ya kina Jomo Kenyatta
Njia ya wasabili ya kuomba uhuru wa kuomba
Njia ya kutegemea adili ya wagandamizaji
Njia ya kuongozwa na masilahi ya ulafi na uroho
Njia ya kukana mapambano ya silaha katika hali ya ufashisti
Mau Mau wakulima na wafanyikazi wa Kenya
Wanaume kwa wanawake wazee kwa vijana
Walichagua barabara ya kimapinduzi ya uhuru
Mau Mau waliyokula kiapo cha ukombozi
Kiapo cha kuwaunganisha na kuwashikanisha kwa mapambano
Mapambano ya kupigania mashamba na uhuru wetu
Mapambano ya kupigania heshima na utu wa mtu mweusi
Mapambano ya demokrasi na haki za binadamu
Mapambano ya kuung'oa ukoloni nchini kwetu
Maelfu kwa maelfu ya wazalendo wa Kenya
Waliyowacha kila kitu na kuitikia mwito
Mwito wa kujitoma milima Kenya na Nyandarua
Mwito wa kusambaa katika miji na vijiji vya nchi yetu
Kuendeleza vita vya kigorila dhidi ya wakoloni na vibaraka wao
Waliyovumilia njaa na kiu na baridi na upweke na dhiki tilatila
Wakajasiri kuwindwa na kukamatwa na kuhamishwa
Waliyokuwa tayari kuvumilia kukamatwa na kufungwa
Mau Mau, maelfu kwa maelfu waliuawa na wakoloni
Mau Mau, ni wangapi mashujaa wetu waliyonyongwa?
Mau Mau, kiboko cha makaburu na mahomugadi
Mau Mau, kwa damu yenu, kwa kujitolea mhanga kwenu
Enyi wananchi wakereketwa wa taifa letu
Kwa msimamo wenu
Kwa mwelekeo wenu
Kwa harakati zenu
Kwa vita sahihi mlivyopigana
Tuko pahali tulipo sasa, hatua kubwa mbele
Ukolonimkongwe haupo tena nasi, mliukwamua Mau Mau
Kwenu Afrika ikapata mfano mzuri wa kuiga
Mfano wa kupigania ukombozi kwa kutumia silaha
Mau Mau, Jeshi la uhuru na Mashamba
Na sisi leo
Lazima tupambane kwa vyovyote vile
Tujikaze kisabuni
Mateso na majaribu ya kila aina
Tunayaona
Na tutaendelea kuyaona
Mau Mau
Vilikuwa vita vya kupigania uhuru wa kitaifa
Vita vya wananchi na wananchi kwa ajili ya wananchi
Navyo vita vya wananchi vilizaa mashujaa wengi, wengi sana
Mashujaa waliyochipuka katika msitari wa mbele
Mashujaa waliyoteuliwa na ari na shauku ya kujitolea mhanga
Kujitolea mhanga kutumikia vita vya ukombozi
Mashujaa waliyodhihirisha ujemedari na uhodari
Wa kuongoza jeshi lililokuwa la wananchi wa Kenya
Mashujaa waliyokuwa mashuhuri katika uwanja wa vita
Kwa usanii wa kuzalisha hila na mbinu za kuwachapa maadui
Mashujaa wa siasa na itikadi ya wanaonyanyaswa
Waliyohamasisha umma kwa maneneo na vitendo vyao
Mashujaa wa kutetea haki na ukweli na masilahi ya wengi
Waliyochagua kuishi maisha ya utu ya kupinga dhuluma
Mashujaa kwa mapenzi ya nchi yetu na ukombozi wake
Kwa maendeleo ya Kenya na furaha ya kila raia
Kwa imani na amani ya wanaonyonywa na kunyanyaswa
Mashujaa waliyokuwa wakipiga konde nyoyo kila wakati
Waliyopambana dhidi ya kulegalega na kukata tamaa
Mashujaa ambao baada ya kukamatwa na wakoloni
Wakiwa mikononi mwa makaburu na mahomugadi
Wakiteswa katika magereza ya wadhalimu wa nchi yetu
Katikati ya ufashisti wa dola la Waingereza
Walivumilia yote kwa ujasiri usiyo na kifani
Walikataa kusaliti kiapo cha kupigania uhuru
Wakadinda kukana vita vya haki vya ukombozi wa Kenya
Wasikubali kutoboa siri wala kusaliti makomredi wao
Na hata waliponyongwa na kuuawa kinyama kabisa
Mashujaa wetu walikufa kwa fahari
Wakawawachia wakoloni na vibaraka wao aibu ya milele
Ni wengi mashujaa wa Mau Mau, wengi sana
Kwani Mau Mau ni wanati, wananchi wazalendo wakereketwa
Mau Mau, ushujaa wa mamilioni
Ya wakulima na wafanyikazi
Wanaume kwa wanawake wazee kwa vijana
Ambao kwa moyo wa harambee uzalendo na kujitegemea
Walifunga sura ya ukolonimkongwe katika nchi yetu
Na sisi leo
Lazima tupambane kwa vyovyote vile
Tujikaze kisabuni
Mateso na majaribu ya kila aina
Tunayaona
Na tutaendelea kuyaona
Kimaathi
Dedan Kimaathi
Dedan Kimaathi wa Waciuri
Mkuu wa jeshi la Uhuru na Mashamba
Kati ya majemedari wa Mau Mau Kimaathi ali ni gogo
Baina ya mashujaa wa uhuru hakika Dedan Kimaathi ni nyota
Nyota iliyoonekana na inayoonekana katika kila pembe ya Kenya
Nyota inayong'aang'aa Afrika kuonyesha barabara sahihi
Barabara ya kimapinduzi ya kuelekea kwa uhuru
Nyota mashuhuri Afrika na hata duniani kote
Kwa wanaonyonywa na kugandamizwa
Oh pande la mwana wa Kenya, ndugu yetu mpendwa Kimaathi
Ni maneno gani tutayatumia ewe mwana wa Waciuri
Hata tukaeleza sifa zako tilatila kwa kikamilifu?
Ninashindwa hata kupata nahau bora
Za kuandika kuhusu Mkuu wa Jeshi la Uhuru na Mashamba
Pengine niseme tu kuwa Kimaathi alikuwa mtu
Alikuwa mtu Kimaathi, mtu kama sisi
Alikuwa na mamaye na babaye na bibiye na babuye
Alikuwa na jamaaze, damuze, kama sisi
Alikuwa na mke, mke aliyempenda sana, tena sana
Kimaathi alikuwa kijana, kijana kama sisi
Kijana aliyetambua jukumu lake kama mwananchi mzalendo
Mtu ambaye alifahamu yu mtu kwa maneno na matendo
Kimaathi, maana ya mapenzi kwa nchi yako na watu wake
Kimaathi, mfano halisi wa ushujaa wa kimapinduzi
Ushujaa wa umma uhodari wa masilahi ya wanaogandamizwa
Kimaathi, twasira na jazanda ya kujitolea mhanga
Kwa uhuru na ukombozi wa kitaifa
Kati ya wasanii wa hila na mbinu ya vita vya kigorila
Kimaathi wa Waciuri anatajika kama sogora mkubwa
Kati ya majina yaliyokuwa yakiogopewa na wakoloni
Jina la Dedan Kimaathi lilikuwa namba wani
Kimaathi aliwafanya makaburu kujikojolea na kujiharia
Wanyonyaji wakashindwa kula manyonyaji yao kwa amani
Wangapi walowezi walifungasha na kuondoka
Kwa kuogopa Kimaathi, asakari hodari wa Mau Mau!
.....ahhhh! lakini nani asiyemfahamu Kimaathi nchini!
Ni mwananchi gani mzalendo ambaye hajui Mau Mau!
Ni historia gani ya Kenya hiyo ambayo haitaji Mau Mau!
Ni mashujaa gani wa Kenya unawajua kama humjui Kimaathi!
Hakika katika kuandika historia sahihi ya taifa letu
Hatutawasamehe kina Ndirangu Mau milele
Kina Ndirangu Mau - mahomugadi waliyomsaliti shujaa wetu
Kina Ndirangu Mau - kina Kenyatta na Moi wenye dola la kisaliti
Kina Ndirangu Mau - wanyonyaji wa wakulima na wafanyikazi
Kina Ndirangu Mau - vibaraka wa mabeberu
Kina Ndirangu Mau - wanaopinga ukombozi wa taifa letu
Tutawasemehe vipi kwa kuendelea kukataa kumzika Kimaathi!?
Mnamo tarehe 18 Februari mwaka wa 1957
Katika Jela ya Nairobi
Dedan Kimathi wa Waciuri, shujaa mkuu wa Kenya
Alinyongwa na wakoloni wa Wingereza
Alinyongwa baada ya mateso ya kifashisti ya kina Ian Henderson
Alinyongwa huku akipambana akiwa na pingu mikononi
Shujaa wa nchi yetu alikufa akipigana
Mwili wa Kimaathi ulitupwa na wakoloni
Katika Jela ya Kamiti
Na hadi wa leo
Mazishi ya Mzalendo Kimathi
Yanangojea kufanywa, tukumbuke
Na sisi leo
Lazima tupambane kwa vyovyote vile
Tujikaze kisabuni
Mateso na majaribu ya kila aina
Tunayaona
Na tutaendelea kuyaona
Mathenge
Stanley Mathenge
Jemedari Stanley Mathenge
Sehemu ya shina na mzizi wa Mau Mau
Komredi mkuu wa Kimathi
Mzalendo Stanley Mathenge
Naye daima hatutamsahau hakika
Kwani yu shujaa wa uhuru wa nchi yetu
Msituni alitambulikana kwa uadilifu na ukakamavu
Daima alikuwa tayari kufa akitetea haki na ukweli
Kwa wakoloni na mahomugadi na wasaliti wote
Mathenge alikuwa hatari kwa usalama
Kwa maaskari wa Mau Mau
Mathenge ali kamanda wa kutegemea
Kwa wananchi wa Kenya
Kina Mathenge ni jazanda la matumaini
Mathenge alikuwa tayari kufa kuliko kusarenda kwa ukoloni
Mashambulizi ya jeshi la kikoloni yalipokuwa mno
Mabomu ya ndege za wakoloni yalipozidi usiku na mchana
Hata yakatisha kugeuza milima Kenya na Nyandarua jangwa
Tatizo la Mau Mau la kukosa silaha za kutosha lilipokuwa mno
Wasaliti walipopenya hadi ndani ya misitu katikati ya Mau Mau
Yasemekana kina Mathenge waliamua kutoka msituni
Kutoka msituni na kukimbilia Kaskazini mwa nchi yetu
Wengine walisema kuwa kina Mathenge walifika Ethiopia
Hatuna hakika, serikali ya mahomugadi ya Kenyatta na Moi
Haina haja ya kujua ukweli - ukweli kuhusu kina Mathenge
Ela ukweli ni kwamba
Mathenge alikataa katakata kuwainulia wakoloni mikono
Alikuwa tayari kufa kuliko kusarenda Mathenge
Popote alipoenda
Alienda akiwa mzalendo wa Kenya
Hakuwacha kuwa shujaa wa umma Mathenge
Kina Mathenge na Mau Mau
Pandikizi za watu
Wazalendo tuna kazi kubwa
Kazi ya kumtafuta Mathenge, kina Mathenge
Na sisi leo
Lazima tupambane kwa vyovyote vile
Tujikaze kisabuni
Mateso na majaribu ya kila aina
Tunayaona
Na tutaendelea kuyaona
Kago
Kariuki Kago
Jemedari Kariuki Kago
Mwana wa maskwata
Maskwata waliyoporwa mashamba yao na walowezi
Mamilioni ya wakulima makabwela wa Kenya
Waliyotimuliwa na masetla wa kikoloni
Kutoka kwa ardhi yao ya jadi
Wakigeuzwa mafukara na walalahoi
Wananchi wasiyo na hata inchi ya nchi yao
Shujaa Kariuki, Kago Kariuki alichukia ukoloni mno
Ali akichemka kwa hasira ghamu na ghamidha
Ali akisisimuka na kutetemeka kwa ghadhabu
Alifahamu uchungu na aibu ya kutawalwa na Wazungu
Akakataa kuketi na kulia na kulalamika bila vitendo
Ndipo kibirikizi cha Mau Mau kilipolia Kago alikisikiliza
Alikisikiliza akajitoma katika msitu wa Nyandarua na silaha
Kuungana na wanaume na wanawake wa vitendo halisi vya uhuru
Katika uwanja wa vita vya kigorila Kago ana sehemu
Alionekana bayana kwa ujasiri na uhodari wake
Alikuwa sogora wa mbinu ya kuvizia na kushambulia ghafla bin vuu
Kina Kago kwa uhodari na ujemedari wao
Waliwaweza wakoloni na dola lao
Mnamo mwaka wa 1954 mwezi wa Machi
Kago, ndugu yetu mpendwa Kago, aliuawa na maadui
Katika msitari wa mbele
Alikufa kifo cha shujaa na bunduki ya haki mikononi
Wakati minara ya mashujaa itakapojengwa
Mwingine utakuwa wa Kago
Na sisi leo
Lazima tupambane kwa vyovyote vile
Tujikaze kisabuni
Mateso na majaribu ya kila aina
Tunayaona
Na tutaendelea kuyaona
Kariba
Kariba (Hituchi Kabutu)
Jemedari Kariba wa kikosi cha Hika Hika
Simba wa Mathira na Tetu
Kariba alikuwa kiboko cha makaburu na mahomugadi wa Nyeri
Aliwasisimua na kuwahamasisha wengi kusimama imara
Katika msitu wa Kirinyaga
Jemedari China
Katika enzi za ushujaa wake
Alimwamini Kariba kama mchapaji kazi ya vita vya ukombozi
Kariba, mfano wa vijana tunaowahitaji leo
Mnamo Oktoba mwaka wa 1954 alikamatwa na polisi wa kikoloni
Kariba akashawishiwa akatishwa akateswa kuteswa
Bali shujaa wa vita vya umma akakataa kukana Mau Mau
Akadinda kabisa kuwalilia na kuwaomba maadui
Kariba asikubali kusaliti vita vya haki vya ukombozi
Siku utenzi wa mashujaa wa uhuru wa Kenya utakaposomwa
Beti kadhaa zitakuwa za Kariba
Mnamo Alhamisi tarehe 6 Januari mwaka wa 1955
Jemedari Kariba
Mkuu wa kikosi cha Hika Hika
Akanyongwa na wakoloni
Mzalendo Kariba
Alichinjwa na wakoloni katika Jela ya Nairobi
Na sisi leo
Lazima tupambane kwa vyovyote vile
Tujikaze kisabuni
Mateso na majaribu ya kila aina
Tunayaona
Na tutaendelea kuyaona
Tanganyika
Muriuki Kimotho - Jemedari Tanganyika
Tanganyika naye ni twasira ya ushujaa na uhodari
Na tena yu kamusi ya maana ya uzalendo na kujitolea mhanga
Akiwa amebaki kiongozi wa kikosi cha Hika Hika
Huko Mlima Kenya
Tanganyika alidhihirisha uongozi thabiti wa ukakamavu
Mashambulizi ya wakoloni na mahomugadi yaliyochacha
Mabomu kutoka kwa ndege za ufashisti wa Wingereza yaliyozidi
Dhiki za maradhi na njaa na baridi zilizoongezeka mno
Ukosefu wa silaha uliyokuwa tabu kubwa kwa Mau Mau
Usaliti wa Jemedari China uliyokuwa pigo kubwa kwa Mau Mau
Haya yote Tanganyika alipambana nayo bila kukata tamaa
Tanganyika alikataa katakata
Kuwacha harakati za ukombozi bila ukombozi
Aligoma kuutambua utawala wa wakoloni katika nchi yetu
Hakukubali kushirikiana na vibaraka wa wakoloni
Alikamatwa mnamo tarehe 10 mwezi wa Aprili mwaka wa 1956
Muruiki Kimotho alikamatwa na kutiwa ndani na wakoloni
Akashawishiwa akatishwa akafanyiwa unyama usiyo na kifani
Bali ndugu yetu akakataa kuwalilia na kuwaomba wakoloni
Tanganyika asikubali hata kidogo
Kujuta kwa kutekeleza jukumu lake la kizalendo
Akashikilia vita vya ukombozi ni vita halali
Mapambano dhidi ya dhuluma ni ya ukweli na haki
Wakati tutakapotunga nyimbo za kuimba sifa za mashujaa wetu
Jina la Tanganyika litasikika kwa fahari katika maghani yetu
Mnamo tarehe 6 mwezi wa Julai mwaka wa 1956
Tanganyika akanyongwa katika Jela ya Nairobi
Muriuki Kimotho akaungana na maelfu ya mashujaa wetu
Waliyotoa maisha yao kuwa matambiko
Ya uhuru na ukombozi wa taifa letu
Na sisi leo
Lazima tupambane kwa vyovyote vile
Tujikaze kisabuni
Mateso na majaribu ya kila aina
Tunayaona
Na tutaendelea kuyaona
Mukami
Alice Mukami
Alice Mukami Kimaathi
Mzalendo Alice Kimaathi
Askari hodari wa Mau Mau
Mukami gorila mashuhuri mijini na vijijini na msituni
Mukami kiongozi wa kikosi kabambe cha wanawake
Mukami na wanawake, wanawake wazalendo wa Mau Mau
Mbiu ya mgambo ilipolia kutangaza vita vya uhuru na mashamba
Vita vya kupambana dhidi ya wakoloni na mahomugadi wao
Mukami hakusitasita aliamua kimoja
Akafuatana na mumewe Kimaathi kwa hiari yake mwenyewe
Akawa sehemu ya maelfu ya wanajeshi wanawake wa Mau Mau
Waliyokuwa sababu ya ufanisi mkuu wa Mau Mau
Mukami alitambua jukumu lake
Kama Mkenya na kama binadamu
Kweli Mukami ni jazanda la ushujaa wa wananchi
Siku ya kuwapamba mashujaa wa uhuru wa Kenya itakapofika
Tutampamba Mukami kwa dhahabu na almasi
Anaishi hadi wa leo Mukami anaishi kwa uzalendo
Serikali ya mahomugadi wa jana na leo inayotutawala
Inaendelea kumnyanyasa mama yetu mpendwa
Inakataa kumuonyesha Mukami kaburi la mumewe Kimaathi
Maadui wakubwa wa uhuru na ukombozi wa taifa letu
Wanaovuruga na kuparaganya historia yetu ya mapambano
Wanaendelea kukana Mau Mau na kina Alice Mukami
Wanaendelea kuwashindilia katika kasumba ya dini
Bali kina Mukami
Hawana haja ya kutambuliwa na wasaliti wa Mau Mau
Wanafahamu
Ingawa juhudi zao ziliung'oa ukolonimkongwe
Mapambano bado yanaendelea
Kwani ukolonimamboleo ungaliko
Mukami, bado kina Mukami wanahitajika
Na watahitajika milele
Na sisi leo
Lazima tupambane kwa vyovyote vile
Tujikaze kisabuni
Mateso na majaribu tilatila
Tunayaona
Na tutaendelea kuyaona
J.M.
Josiah Mwangi Kariuki
Mzalendo Josiah Mwangi Kariuki
Mau mau kizuizini
Sauti ya Mau Mau bungeni
Jina linaloendelea kuufafanua u-Mau Mau
U-Mau Mau katika enzi za ukolonimamboleo
Josiah Mwangi Kariuki, Mau Mau kizuizini
Wakati kibirikizi cha Jeshi la Uhuru na Mashamba kilipolia
Kilipolia kuwaita wazalendo wajitokeze wawajibike
Wawajibike kwa ajili ya uhuru na ukombozi wa Kenya
J.M. hakusitasita wala hakulegalega
Alijitokeza kimoja kutekeleza jukumu lake
Jukumu lake kama mwananchi na mzalendo mkereketwa
J.M. akawa sehemu ya Mau Mau
Alipotiwa mbaroni na kufungwa kizuizini
Pamoja na mateso yote aliyoteswa
Pamoja na vitisho vyote alivyotishwa
Pamoja na vishawishi vyote alivyoshawishiwa
Pamoja na unyama wote waliyofanyiwa wafungwa wa kisiasa
Pamoja na magumu yote waliyoyakula Mau Mau kizuizini
JM alikataa kabisa kukana mapambano ya uhuru
J.M. alidinda wakati wote kusaliti Mau Mau
Asikubali hata kidogo kujuta kwa msimamo aliyouchukua
Gerezani akawa taswira ya matumaini na kupiga konde moyo
Na akatoka kizuizini akiwa mzima kama kigongo
Tayari kuendelea na mapambano ya uhuru kamili
Mwaminifu kwa maadili ya Jeshi la Uhuru na Mashamba
J.M. akawa sauti madhubuti ya kusema
Hatukupigania uhuru ili tuingie nafasi ya wakoloni
Hatukupambana ili kunyang'anyana mashamba na maploti
Hatukuingia msituni ili kuteseka na kufa
Kwa ajili ya mahomugadi wa jana na leo
Wala hatukufungwa na kula ngumu
Ili kuleta mfumo wa unyonyaji wa mtu kwa mtu
Hatuwezi kujivunia Kenya ya mamilionea kumi
Na maskini milioni kumi
Tulikataa unyonge wa kunyanyaswa na kina Lodi Delamare
Na huu wa kugandamizwa na kina Jomo Kenyatta hatuutaki pia
Josiah Mwangi Kariuki
Pamoja na utajiri wake wote
Akajipiga kitanzi cha kitabaka
Na kuwa upande wa wengi wanaonyonywa
Bungeni akawa mwakilishi halisi wa mamilioni ya Wakenya
Kwa msimamo wake akawa sumu
Kwa utawala wa kisaliti wa Kenyatta
Mkenya kwa kila hali
Daima aliulani ukabila na ubaguzi wa rangi
Komredi wa wafanyikazi siku zote
Aliupinga mfumo wa ubepari
Mwandishi wa uzalendo wa Mau Mau
Josiah Mwangi Kariuki alipendelea uchumi wa kisoshalisti
Alipambania uchumi wa kitaifa
Wa haki na unaojitegemea na kujiendeleza
Ndiyo kwa maana serikali ya kigaidi ya Kenyatta na kanu
Mnamo mwaka wa 1975
Ilimuua J.M.
Kinyama kabisa
Na kutupa mwili wake
Katika msitu wa Ngong’ ili uliwe na fisi
Lakini hata fisi wenyewe
Walimheshimu J.M. kwa ushujaa wake
Fisi wakakataa kabisa kumla ndugu yetu mpendwa!
Maiti ya Kariuki yakapatikana
Uhalifu wa Kenyatta ukabainika hata zaidi
Serikali ya wasaliti ikatingishika
Wingu la huzuni likafunika nchi yetu
Mvua ya machozi ya majonzi ya wazalendo
Ikanyesha Kenya nzima na hata Afrika Mashariki
Kilio cha Wakenya kikasikika duniani kote
Mzalendo Josiah Mwangi Kariuki
Tukamfanyia mazishi ya shujaa wa umma
Tukamzika komredi wetu kwa vifijo na ndremonderemo
Na tukaamua kutowasamehe wauwaji wake milele
Na tarehe 3 Machi
Tukasema ni siku ya J.M.
Josiah Mwangi Kariuki
Na sisi leo
Lazima tupambane kwa vyovyote vile
Tujikaze kisabuni
Mateso na majaribu tilatila
Tunayaona
Na tutaendelea kuyaona
Tusisahau enzi za makumi ya themanini
Nyakati za ukolonimamboleo
Mfumo wa usaliti wa Moi na kanu
Udikteta ulipotia fora katika nchi yetu
Tukawa ja tu chini ya ufashisti
Mipango halisi ya dola la imla
Kuhofisha na kushurutisha
Na kuamrisha na kugandaniza na kunyanyasa
Udhalimu ukahalalishwa na kurasimishwa kikatiba
Mfumo wa chama kimoja cha KANU cha kanu
Sheria za uchochezi na uhaini
Zikafunguliwa dhidi ya raia
Haki ikikanyagwa na kuvunjwa kiholela
Ukweli ukipakwa matope na kudharauliwa
Utu wa mtu ukipuuzwa na kufanywa si kitu
Wenye nguvu za dola wakigeuka wanyama
Hayawani dhidi ya binadamu na ubinadamu
Mahakama yakigeuzwa kuwa ya bandia
Kenya ikawa chini ya mfumo wa imla kisheria
Chama cha kanu cha kutawala kwa tuteni
Chama cha kupinga uhuru na maendeleo
Chama cha wanyonyaji wezi na wafisadi
Chama cha vibaraka na vibarakala
Chama cha genge la wajinga na wakora
Chama cha waporaji wa mali ya umma
Chama cha Kanu
Kanu ya Moi
Moi wa kufuata nyayo za Jomo Kenyatta
Kenyatta aliyesaliti uhuru wa taifa letu
Kwa ulafi wa pesa na unyakuzi wa mashamba
Kwa uroho wa mali za duniani
KANU ya kanu
Mtu mmoja akitawala Kenya
Kana kwamba ni shamba lake binafsi
Akinyakua kila alichokitamani
Pamoja na wanawe na vibaraka wake
Ikawa lazima kila raia awe chini ya chama cha Kanu
Vyombo vya dola vikitumika
Kuulinda na kuuimarisha utawala wa mabavu
Polisi na mahakimu na magereza na utawala wa mikoa
Wakitekeleza amri za kishenzi na kikatili
Amri za kupambana dhidi ya uhuru wa wananchi
Amri za kupinga na kukataza haki za binadamu
Amri za kutekeleza sheria za katiba ya udhalimu ya kikoloni:
Kusiwe na chama kingine isipokuwa cha kanu
Kusiwe na siasa zozote isipokuwa za kanu
Kusiwe na viongozi wowote isipokuwa wa kanu
Kusiwe na mikutano yoyote bila ruhusa ya machifu wa kanu
Kusiwe na uchaguzi wowote isipokuwa wa viongozi wa kanu
Rais Moi akiwa jitu shetani bin ibilisi
Kusiwe na rais yoyote isipokuwa Moi
Kusiwe na habari zozote bila kutaja Moi
Kusisifiwe mtu yoyote mwingine ila Moi
Kila kitu kiitwe Moi au Kenyatta
Kwaya na ngoma zote ziimbe na kumsifu Moi
Maombi yote yaombewe Moi
Kusiwe na maswali yoyote ila kutii amri
Amri kutoka kwa Moi
Ikawa kukosoa rais au serikali
Ni uchochezi ni uhaini
Kuukemea ufisadi na ubepari na ubeberu
Ni kosa kubwa kuliko unyang’anyi
Tukawa kama watumwa
Katika nchi yetu wenyewe
Usiku na mchana
Tukisakwa na kuwindwa
Tukiishi kwa hofu na wasiwasi
Tukikamatwa kuteswa kushtakiwa na kufungwa kiholela
Wasomi wazalendo wakifutwa kazi na kuwekwa vizuizini
Viongozi wa wanafunzi wazalendo wakifukuzwa vyuoni
Migomo ya wafanyikazi
Ikivunjwa kwa mitutu ya bunduki
Usanii wa kizalendo ukipigwa vita mbele na nyuma
Majasusi wakiwekwa kila pahali
Mijini na mashambani
Afisini na viwandani na mitaani
Kazi kubwa ya polisi
Ikawa ni kupambana dhidi ya waasi
Waasi wa uongozi wa giza na kifo
Waasi wa utawala wa Moi na kanu
Waasi wa mfumo wa ubepari na ukoloni mamboleo
Waasi wa utamaduni wa hofu na kimya
Waasi wa maadili ya kuabudu pesa na mali
Waasi wa nyanyaso na gandamizo
Waasi wa ufisadi na usaliti wa taifa
Waasi wenye kudai mageuzi
Mageuzi ya kuondoa mfumo wa ubepari
Mageuzi ya kuleta uhuru na demokrasi
Mageuzi ya kujenga mfumo wa usoshalisti
Magereza yakajaa wazalendo na wanamapinduzi
Wengi wakisukumwa uhamishoni
Kwa kuzidi kwa nyanyaso
Uchumi ukazidi kuporomoka
Kwa kuparaganywa, kuhujumiwa na kuporwa kiholela
Uporaji wa mashamba na maploti na mashirika ya umma
Ukawa sehemu ya maisha ya kila siku
Barabara zikinyakuliwa
Misitu ikinyakuliwa
Pwani zikinyakuliwa
Mito ikinyakuliwa
Vinamasi vikinyakuliwa
Maziwa yakinyakuliwa
Visiwa vikinyakuliwa
Viwanja vya michezo vikinyakuliwa
Shule zikinyakuliwa
Makaburi yakinyakuliwa
Hata vyoo vya umma vikinyakuliwa
Kisibaki kisichokuwa na hatari ya kunyakuliwa
Unyakuzi unyakuzi unyakuzi unyakuzi
Ukifukarisha wakulima makabwela mashambani
Na kuzidisha mitaa ya mabanda mijini
Ukosefu wa kazi ukizidi na kuzidi na kuzidi
Bali
Upinzani kwa upande wake
Ukakua na kukua na kukua na kukua
Wala usisite kukua
Kila siku ukakua
Ukakua vyuoni na viwandani pia
Mijini ukakua na mashambani vilevile
Wazalendo wakikutana
Hadharani na mafichoni
Wakijipanga na kujizatiti
Mara juu kwa juu na mara chini kwa chini
Wakajitolea mhanga
Kupigania ukombozi
Na sisi leo
Lazima tupambane kwa vyovyote vile
Tujikaze kisabuni
Mateso na majaribu tilatila
Tunayaona
Na tutaendelea kuyaona
Ndiyo, tusiwasahau wazalendo
Waliyojitolea mhanga kufa na kupona
Kwa udi na uvumba
Kupambana dhidi ya udikteta wa Moi na Kanu
Na kudai uhuru na demokrasi na Katiba ya Kenya
Wakipambania mfumo wa ujamaa
Hawa ni mashujaa wa kweli wa uhuru
Wanastahili kuandikwa kwa historia
Tuwaonee fahari milele na milele
Kwa kuvumilia mengi magumu na mazito na machungu
Kwa ujasiri na ukakamavu
Kwa kupambana pasina kukata tamaa
Wakishikilia nyoyo za matumaini
Huku wakikumbuka Mau Mau
Wakaleta ushindi dhidi ya imla hatimaye
Utawala wa mfumo wa chama kimoja cha kanu
Ukaanguka ukachunuka ukaondoka ukahiliki
Na sisi leo
Lazima tupambane kwa vyovyote vile
Tujikaze kisabuni
Mateso na majaribu tilatila
Tunayaona
Na tutaendelea kuyaona
December Twelve Movement - DTM
Mwakenya
Wali ni wazalendo na wanamapinduzi
Vijana na wazee
Wanafunzi wa vyuo vikuu
Walimu wa taasisi mbalimbali
Wafanyikazi na wakulima
Kutoka sehemu mbalimbali za Kenya
Ambao waliamua kuunda chama
Chama cha chini kwa chini
Wakiandika kuchapisha na kusambaza Pambana
Pambana kutoka Wangige Kibichiku na Momoto
Pambana gazeti la DTM
Pambana sauti ya mapambano
Mapambano dhidi ya utawala wa imla
Mapambano dhidi ya ufisadi na uporaji wa mali ya umma
Mapambano dhidi ya ubepari na ubeberu
Mapambano ya kupigania mfumo wa kisoshalisti
Pambana jarida la uchochezi
Kuwachochea umma unaonyonywa na kunyanyswa
Uamke uungane ushikane utende
Wakenya wasikubali kugawanywa kikabila
Pamoja wapambanie ukombozi wao
Watambue msingi wao wa kitabaka
Waishikilie itikadi ya ukombozi kamili
Itikadi ya kisoshalisti
Kuwachochea wanafunzi na wasomi
Wagomee utawala wa kijinga na kimabavu
Kuwachochea wafanyikazi
Wajizatiti wapiganie masilahi yao na ya jamii
Kuwachochea wakulima makabwela na maskwata
Wadai mashamba na maploti
Kuwachochea wadhulumiwa wote
Wachukie dhuluma na wadhalimu
Na Mpatanishi
Kuli na Mpatanishi pia
Gazeti la wanachama wa DTM
Mpatanishi gundi la wanachama
Mpatanishi kuwapatanisha wanamapinduzi
Kutoka kila sehemu za nchi yetu
Mpatanishi kuleta umoja wa wanamapinduzi
Mpatanishi kujadili nadharia na itikadi
Mpatanishi kusambaza elimu ya kikomunisti
Mpatanishi kuzatiti na kupanga mbinu na hila
Mpatanishi siri ya DTM
Wanachama wakichangia Pambana na Mpatanishi
Kila mwanachama akitoa kwa harakati
Asilimia fulani ya mapato yake
Si wafanyikazi si wakulima si wanafunzi
Kila mtu alitoa kile alichokiweza
Kuyadhamini mapinduzi
Kili ni chama cha wanachama kwa hali na mali
Watu wazuri sana tena waadilifu
Waliyouchukia ukabila na ubaguzi wa aina yoyote ile
Waliyotambua jukumu lao la kihistoria
Na kutenda ipasavyo
Waliyotambua ukweli halisi
Mfumo wa udhalimu hautaondoka wenyewe
Ni mpaka uondolewe
Uondolewe kwa mipango na mapambano
Mapambano ya wazalendo na wanamapinduzi
Yaliyoukosesha usingizi
Utawala wa Moi
Ndipo naisifu DTM pamoja na Mwakenya
Nasema historia yake
Nikiimba sifa za mashujaa wake
Maana ni jukumu langu
Kwani historia sahihi ya mapambano ya uhuru
Haitaandikwa na wasaliti wa jana na leo
Mashujaa wa kweli wa nchi yetu
Hawatatambuliwa na serikali ya wasaliti
Na hakika mashujaa wa umma
Wanastahili kukumbukwa
Tuwaonee fahari na kuwasifu
Kwani ni mfano mwema wa kuiga
Tena ni ngome ya mtima wa matumaini
Na tochi ya kuangazia leo
Na pia kumulika siku zijazo
Ndiyo
Tuwakumbuke
Mashujaa wa nchi yetu
Wazalendo halisi wa Kenya
Jinsi walivyokuwa wamejitolea mhanga
Kupambania uhuru na ukombozi wa nchi yetu:
Na sisi leo
Lazima tupambane kwa vyovyote vile
Tujikaze kisabuni
Mateso na majaribu ya kila aina
Tunayaona
Na tutaendelea kuyaona
Mwandawiro Mghanga
Jela Kuu ya Kibos Aprili 6 1988
Mnafiki
uwongo wako!
hata kama ni kweli
ulipigania uhuru
hata kama ni hakika
ulikuwa kwa Jeshi la Uhuru na Mashamba
hata kama ulisema nini na kufanya kitu gani
dhidi ya ukolonimkongwe
ikiwa sasa wewe ni msaliti
ikiwa wakati huu u kibaraka cha mabeberu
ikiwa leo wewe ni mnyonyaji
kama u mbakuzi wa mashamba na maploti
endapo unaunga mkono mfumo wa unyonyaji wa mtu kwa mtu
ikiwa unadai kuna uhuru Kenya leo
hakika kabisa wewe si shujaa wa wananchi
wala usifikiri u mzalendo hata kidogo
kwani ulafi wako
tamaa ya mali na pesa
ubinafsi
unafiki na ubarakala wako
umefuta historia yako safi ya jana
kweli huwezi kutudanganya tukadanganyika
wala huwezi kusema tukakusikiliza
katika historia ya leo ya nchi yetu
wewe si rafiki wa mapambano ya ukombozi wa kijamii
leo umegeuka kuwa adui, unapinga maendeleo ya nchi yetu
kwa kuwa umekubali kuwa mbwa wa wakolonimamboleo
kwa sababu unazungumza lugha ya wagandamizaji
madhali unatetea mfumo wa ubepari
maana leo u fisi na nguruwe
maadamu sasa u sawa na kupe na kunguni
kwa vile u malaya mkubwa siku hizi
shujaa wa kweli wa umma
mzalendo halisi
husafiri hadi mwisho wa safari
na safari yetu ya mapambano bado ingaliko
haijafika mwisho wake safari yetu ya uhuru na maendeleo
kwani ukolonimamboleo ungaliko katika nchi yetu
wananchi tunaumizwa na udikteta wa kanu
ingawa bendera inapepea uhuru wenyewe bado
kumbe wewe ulikuwa ukipambania tumbo lako tu
kumbe nia yako ilikuwa kuchukua nafasi ya mkoloni
tulikataa unyonge wa kunyanyaswa na Waingereza
unafikiri tutaikumbatia aibu
ya kudhulumiwa na Wafrika wenzetu?
shetani mkubwa wewe!
msaliti unayechafua jina safi la Mau Mau!
mzandiki!
Mwandawiro Mghanga







