On the 24th and 25th of May, 2014, Kenyans and fellow Africans from all walks of life will converge at the Kenyatta International Conference Centre (KICC) Auditorium to commemorate the 51st anniversary of the Africa Liberation Day (ALD), with a symposium on the 24th of May, starting 10:30am-6:00pm, where among other topics in discussion will be the Decolonisation of Western Sahara, Resolving Wars on the continent, African Unity and the Role of Women in the Pan-Africanist struggles. The theme of this year's ALD is: "PanAfricanism-We Must Dare to Invent the Future" by Thomas Sankara.
There will be an open concert at the KICC courtyard starting at 1:00pm on the 25th of May, with performances from many progressive and conscious artists including Eric Wainaina, Afrizzo Band (Hellen Mtawali),Dr. Dan,Juliani, Sarabi Band, Maumau Vibrations (Ndungi Githuku), Grand Master Masese, Ukoo Flani, Vitalii (from Tanzania), Lam (from South Sudan), Sam Ondieki among many others.
Entrance for both events is free, open to all, and the Social Democratic Party is encouraging all its members and cadres to participate in this very important event on the Party’s calendar.
Below are Four Powerful Poems by Comrade Chairman Mwandawiro Mghanga,dedicated to this year’s ALD, that capture the spirit of African Liberation and Struggles.
Benedict Wachira – Secretary General
22nd May 2014
Hebu viongozi niwasifu, wa kimapinduzi Afrika
Kwameh Nkuruma namsifu, ambaye Ghana alizalika
Na tena alikuwa marufu, kila taifa la Afrika
Kwameh ali jabali arifu, la ukombozi wa Afrika
Alikuwa akituarifu, haja ya umoja Afrika
Na alitenda mambo sufufu, ya ujamaa Afrika
Nkuruma alipoondoka, Ghana bepari wakachukua
Kuna Sekou Ture sikia, nchi ya Guinea ilitupatia
Wafaransa kumsikia, ah! wali wakijikojolea
Nkuruma alipomjua, komredi akajipatia
Na Ghana walipompindua, Conacry alikimbilia
Na pamoja wakapigania, Afriika kujikomboa
Ujamaa wakapambania, Guinea hata Afrika pia
Sekou alipotuondokea, Guinea ikatuharibikia
Madibo Keita nakwambia, Afrika alipigania
Na Mali alipozalikia, jina lake wanajivunia
Ni mzalendo alobobea, tena wa umma kupigania
Ukoloni aliuchukia, hata Kwameh alimtambua
Mali ya nyingi historia, pia Madibo aliichangia
Ujamaa aliwatakia, Wafrika kuushikilia
Ela alipoaga dunia, na Mali ikapotea njia
Naye Nyerere wa Tanzania, ni Mwafrika anosifika
Uhuru aliupigania, wa Tanganyika na Afrika
Ujamaa alizingatia, ni ukombozi wa Wafrika
Siasa ya kujitegemea, aliisema na kuandika
Mwalimu alitukariria, haja ya umoja Afrika
Na elimu ya kujikomboa, na Kiswahili kikajengeka
Nyerere alipoondoka, walochukua ni matapeli
Kuna Amilcar Cabral, alikuwa mwanamapinduzi
Wafrika walimkubali, kuwa shujaa wa ukombozi
Guinea Bissau ni yake asili, bali Afrika alienzi
Ujamaa mfumo halali, alifunza mwanamapinduzi
Alikuwa mwalimu kamili, wa nadharia ya mapinduzi
Hakuwa wa kuabudu mali, alipenda haki na mapenzi
Bali alipouawa mpenzi, na Guinea Bissau ikapotea
Agostino Neto sikia, ni mwanamapindizi Angola
Uhuru aliupigania, huku ujamaa akilola
Mabeberu walimchukia, wakamfanyia kila hila
Bali Neto aliendelea, hakukatishwa tama na dhila
Mashairi alituwachia, ya uhuru na haki kulola
Umoja Afrika kukua, Neto alipinga ukabila
Lakini Neto alipolala, na Angola kombo ilienda
Samora Macheli nampenda, ni Msumbiji alizaliwa
Na Afrika aliipenda, na pia siasa za usawa
Ndiyo mana jeshi wakaunda, la Msumbiji kuikombowa
Ndipo vita walipovishinda, ujamaa ukanza kukuwa
Vyema mambo yakaanza kwenda, mfumo wa utu wa usawa
Kusini Afrika akenda, kuchangia nchi kuzikombowa
Ela Samora alipowawa, Msumbiji huna mwelekeo
Na hayo hayakuanza leo, tukumbuke Kenya mashujaa
Mau Mau hadi hivi leo, twakumbuka waliwasha taa
Afrika kwenda mbiombio, kwa ukombozi wa kisilaa
Siasa za kimaendeleo, za utaifa uje kukaa
Hii hali iliyoko leo, wengi maisha ya kalabaa
Mau Mau ilipinga hayo, wao ni mfumo wa kufaa
Bali bado kale wanakaa, na kupambana wamesimama
Mandela ni shujaa mwadhama, mtu mwema sana duniani
Ni kiongozi mwenye hekima, ali marufu ulimwenguni
Tangu ujana hadi uzima, kwa uhuru au kifungoni
Haki Mandela alitazama, na usawa kweli na amani
Alikuwa mfano mwema, kote na Afrika Kusini
Alitakia wote salama, akipigania maskini
Tulipomueka kaburini, mafisi wa ANC tayari
Na pia huko nchi ya Misri, kuli na kiongozi hodari
Tena alikuwa mashuhuri, kupinga ubeberu kwa ari
Afrika wende ubepari, uhuru wapate amfari
Mashariki ya Kati uhuri, Abdi Naser alikariri
Mfumo ujamaa Misri, mwanapinduzi alihubiri
Kwa Naser Afrika nzuri, ni muungano kuwa tayari
Ela alipokufa si siri, imeenda kikombo Misri
Na huko nchi ya Algeria, Ben Bela ali ni hodari
Nchi yake aliipambania, na wazalendo majemedari
Mashujaa wa Algeria, waliupigania uhuri
Wafaransa wakakimbia, wakakimeza chao kiburi
Afrika alifikiria, huku akipinga ubepari
Ukombozi alisaidia, kwa silaha na kwa kila hari
Bali alipowekwa kwa kaburi, Algeria ni ubepari
Afrika ni kweli si siri, unazoroteka uongozi
Watawalao ni mabepari, watu wasojali mapinduzi
Watu walafi wenye kiburi, wasiyo na utu na mapenzi
Wanaozalisha ufakiri, kwa sera katili za kishenzi
Ndiyo, kwa heri ama kwa shari, lazima tulete uongozi
Wa kupambana na ubepari, historia nzuri kuenzi
Kuwa mapinduzi endelezi, tujenge vyama vya mapinduzi
Mwandawiro Mghanga, Kahawa Sukari, Februari 5 2014
Maliasili za Afrika!
Afrika rasilimali, ni bara limebarikiwa
Madini ni kila pahali, hata kawi tumejaliwa
Na misitu pia ni mali, kwa maumbile tumepewa
Tuna bahari kwa maili, maliasili zimejawa
Utajiri tumejaliwa, na Afrika ni fukara!
Wafrika ni mafukara, na tunazo maliasili
Kutoka pwani hadi bara, tilatila maliasili
Tunapigwa kama mpira, na ni zetu maliasili
Tunaporwa maisha bora, tukiporwa maliasili
Zimejaa maliasili, bali ukiwa unakua!
Ukiwa umetuzidia, na tunazo maliasili
Ulaya wanafaidia, kutokana na zetu mali
HataUchinana India, wanazijasiriamali
Amerika washikilia, kutupora maliasili
Hatuoni cha afadhali, Wafrika ni masikini!
Tunabakishwa masikini, na tuna mzo utajiri
Mali za chini ardhini, tilatila za kila mbari
Zinaenda ughaibuni, kuzalishia utajiri
Sisi twatoa mchangani, kuwapatia mabepari
Tunabaki na ufakiri, Afrika tunaumia!
Afrika tunaumia, tunabaki ’kusaidiwa’
Wageni wanatutumia, maliasili twaibiwa
Na huku wakituibia, viongozi wanatumiwa
Mabepari wafurahia, na umma unasalitiwa
Maliasilitwaibiwa, usalitiwaviongozi!
Usaliti wa viongozi, wanatuuza Wafrika
Ulafi wao viongozi, wa mabeberu vibaraka
Walimi na wafanyikazi, maisha yamejaa shaka
Maliasili ni machozi, badala ya kuwa baraka
Uongozi wa vibaraka, maendeleo unapinga
Maendeleo unapinga, wa vibaraka uongozi
Tunafanywa watu wajinga, na wa ughaibuni wezi
Mana viongozi wajinga, wanatuuza waziwazi
Uhuru wetu wakipinga, tukililia ukombozi
Imekuwa mali ya wezi, maliasili Afrika!
Maliasili Afrika, Wafrika wazimiliki!
Chumi zipate kufufuka, za kuokoa halaiki
Tuwaondoe vibaraka, tuwe na mfumo wa haki
Ikiwa si kwa Wafrika, bora mchangani zibaki
Badala fukara kubaki, tukiporwa rasilimali!
Lazima tuseme ukweli, tunahitaji mapinduzi
Tutumie zetu akili, tusifaidi mabazazi
Watupore rasilimali, na tukiwa wafanyikazi
Watunyonye kwa zetu mali, kwa usaliti uongozi
Lazima yawe mapinduzi, Afrika inahitaji!
Mwandawiro Mghanga, Kahawa Sukari, Machi 18 2014
Swala la Uongozi Afrika
Ni swala nyeti uongozi, Kenya yetu na Afrika
Ili tupate ukombozi, uhuru uweze kufika
Maongozi na uongozi, ni lazima kubadilika
Mana ni jambo lilo wazi, bara letu lafilisika
Kwa kuwakosa viongozi, ambao wanahitajika
Twaongozwa na mabazazi, wasaliti na vibaraka
Tunahitaji mapinduzi, viongozi kujipatia
Viongozi kujipatia, ni shabaha ya mapinduzi
Umma wanaofikiria, binadamu wenye mapenzi
Haki wanaozingatia, wa kuondoa ubaguzi
Wa ukweli kushikilia, wajibikaji na uwazi
Ambao watu wakilia, na waohutoa machozi
Na siwahalifu sikia, kama waleo majambazi
Lazima tutafute njia, tupate viongozi wema
Tupate viongozi wema, ilitupate endelea
Sababu leo tumekwama, kwahakika tumepotea
Kwa maongozi ya dhuluma, ufisadi ulokolea
Viongozi bila heshima, kazi yao ni kunyakua
Ni mafisi ninaosema, wako kujilimbikizia
Hata taifa likizama, hawajali nakuambia
Wanauza wao mama, hawa ni viongozi gani?
Waabudu pesa mashetani, ndiyo viongozi wa leo
Ni watu mfano majini, wanyama viongozi hao
Wametufanya masikini, tuyakatae mambo yao
Ya ubepari ukoloni, twangushe na mfumo wao
Tuwang’oe uongozini, ndiyo kuwe maendeleo
Tujiulize ni kwa nini, bado tunachagua wao!
Tufikirie kwa makini, hujaje wawe viongozi?
Tunahitaji mapinduzi, sisi wenyewe sikia
Wenyewe twachagua wezi, nakisha huku tunalia
Au tunafanya upuzi, chaguzi kutozingatia
Sharti tuifanye kazi, ni sisi tutajikomboa
Ikiwa njia niuchaguzi, tupige kwa kufikiria
Kama njia ni mapinduzi, tukubali kujitolea
Mana swala la uongozi, ni swala la ukombozi
Mwandawiro Mghanga, Dream Hotel Ngara, Alhamisi Mei 15 2014
Ukombozi ni Mapambano
Kila siku tunalilia, kupata mfumo mzuri
Wa haki kwa kila raia, salama na kila la heri
Utu wa mtu kujalia, na kuondoka ufakiri
Hata ukabila pia, ukagura na zake shari
Usawa wa kijinsia, na kujali kila umri
Ni ndoto tunajiotea, mambo mema kuyafikiri
Bali bila kupambania, ndoto zetu hazijiri
Kwa hakika hayatajiri, pasipo kupambania
Hadi tuwe na uhodari, kwa uwoga kuuondoa
Bila kujiweka tayari, tutakayo kupigiania
Tutabaki kwa ufakiri, katika ndoto kuselea
Kila siku tunafikiri, na ufisadi wendelea
Tupambanie nakariri, ndio yawe tunolilia
Ili mambo yawe tayari, kujizatiti fikiria
Tumejaza Kenya tabia, ya kukaa na kufikiri
Sera nzuri kujipangia, na kujichorea mazuri
Kisha pia kuombea, Mwenyezi tukitafakari
Misikitini kuswalia, na makanisa forofori
Kwa maombi kutujalia, bila sisi kutia ari
Ni bure hayatakua, bila juhudi hayatajiri
Haki ni kupigania, na hili si jambo la siri
Hapatii bure bepari, haki kwao wafanyikazi
Hana huruma mwaajiri, mabepari ni mabazazi
Kujiongeza utajiri, kwa kunyonya wafanyikazi
Hajaye ukue mtaji, mengine kwake ni upuzi
Alazimishwe bepari, na vita vya wafanyikazi
Kwa umoja wakiwa hodari, haki zao watamaizi
Ni sharti tuwe tayari, kupigania ukombozi
Na mapambano ni kazi, ni juhudi za kujitolea
Chama kuoganaizi, na mikakati kupangia
Malengo bora kumaizi, na uwoga kuuondoa
Tukijizatiti kwa kazi, hatimaye tutatoboa
Ni kama vya kimapinduzi, vita ninavyosimulia
Kuiondoa simanzi, ya nyanyaso kuvumilia
Ni kuwa tayari kwa kazi, jambo hili nalirudia
Tukumbuke historia, ili ukweli kuujuwa
Mwanzo wakituvamia, vita vikubwa vilikuwa
Wakoloni waliwajua, wazalendo waliyokuwa
Na ili uhuru kungia, Wakenya kujikombowa
Ilibidi kupigania, kwa mapambano kunyakuwa
Na hata demokrasia, ilibidi kupambaniwa
Mana bila kujitolea, tutagandamizwa milele
Hali itawa vilevile, tukingojea wa bwerere
Tulalamike na tulile, bila kupigania ni bure
Watatukalia milele, tusipotoka na mishare
Tukitaraji kwenda kule, kufika kwa jamii shware
Ni lazima huku na kule, chama kijae forifore
Haki haziji kwa fadhile, au huruma za bepare
Ni tangu zamani za kale, haki haziji burebure
Kwa beti hizi nakaririle, uhuru ni kuwa tayare
Mwandawiro Mghanga, Kahawa Sukari, Januari 24 2014







